TAARIFA YA AWALI YA MATOKEO NA MAPENDEKEZO YA WAANGALIZI WA UCHAGUZI WA KIMATAIFA WA IRI/NDI – UCHAGUZI MKUU WA KENYA AGOSTI 9, 2022

Taarifa hii ya awali inatoa matokeo na mapendekezo ya awali ya  pamoja  ya wajumbe wa Taasisi ya Jamuhuri ya Kimataifa  (IRI) na Taasisi ya Demokrasia ya Kitaifa (NDI) kuhusu uangalizi wa uchaguzi mkuu wa Kenya wa 2022 kufuatia upigaji kura na kuhesabiwa mnamo tarehe 9 Agosti.

Siku ya uchaguzi,  NDI/IRI walishirikiana kutuma wajumbe 30 wa kimataifa ambao hawakuwa na mwegemeo wowote wa kisiasa kutoka nchi 13 wakiongozwa na: Mheshimiwa Joaquim Chissano, Rais wa zamani wa Jamhuri ya Msumbiji; Bi. Donna Brazile, Mjumbe wa Bodi ya NDI na aliyekuwa Kaimu Mwenyekiti wa Kamati ya Kitaifa ya Kidemokrasia (DNC); Mheshimiwa Randy Schuenemann, Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya IRI; Balozi Johnnie Carson, Mjumbe wa Bodi ya NDI , Katibu Msaidizi wa zamani wa Masuala ya Afrika,  Makamu wa Rais wa programu IRI , Bw. Scott Mastic na Mkurugenzi wa Kimataifa wa Uchaguzi wa NDI, Bw. Richard Klein.

Wajumbe hawa walizuru Kenya kuanzia tarehe 4-11 Agosti 2022. Maangalizi yao yalichangiwa na matokeo na mapendekezo ya tathmini mbili za ngazi ya juu  za kabla ya uchaguzi uliofanywa mwezi wa Mei na Juni, mtawalia. Aidha, wamenufaika kutokana na uchanganuzi unaoendelea wa mchakato wa uchaguzi uliofanywa na timu ya wachanganuzi wa muda mrefu walioko Nairobi tangu mwanzo wa Mei. Wajumbe hao walifanya shughuli zao kwa mujibu wa sheria za Kenya na vile vile, Azimio la Kanuni za Uangalizi wa Uchaguzi wa Kimataifa na kwa ushirikiano na jumbe zingine za kimataifa za waangalizi wa uchaguzi pamoja na waangalizi wa kiraia. Matokeo ya awali ya wajumbe na mapendekezo yanatolewa kwa kurejelea viwango vya kimataifa na kikanda vya chaguzi zinazoaminika, ikiwa ni pamoja na Mkataba wa Afrika wa Demokrasia, Uchaguzi na Utawala, pamoja na mfumo wa kisheria juu uchaguzi nchini Kenya.

Lengo la wajumbe wa IRI na NDI ni: kueleza nia ya jumuiya ya kimataifa na kuunga mkono. ushirikishi, uwazi, uwajibikaji na amani nchini Kenya; kutoa taarifa sahihi zisizo na upendeleo na kwa wakati unaofaa kuhusu mwenendo wa uchaguzi wa Kenya wa 2022; na kutoa mapendekezo ambayo yanaweza kutekelezwa kwa kuzingatia utendakazi unaokubalika kimataifa ili kuimarisha uaminifu wa michakato ya uchaguzi nchini Kenya. NDI na IRI wanatambua kuwa ni wakenya ambao hatimaye watabainisha uaminifu wa uchaguzi wao.  

Wajumbe  hao walikutana na washikadau mbalimbali wa uchaguzi, wakiwemo: Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), vyama vya kisiasa, mashirika ya kiraia, makundi ya waangalizi wa kiraia, mahakama na watendakazi wa vyombo vya habari. Timu za wajumbe zilitumwa kwa kaunti 12 kati ya 47 kote nchini Kenya, zikiwakilisha anuwai ya nchi na ambapo waliangalia michakato ya ufunguzi, upigaji na kuhesabu kura. Shughuli zote ziliendeshwa kwa misingi isiyoegemea upande wowote na bila kuingilia mchakato wa uchaguzi. Wajumbe hao wanashukuru   mapokezi mazuri na ushirikiano waliopokea kutoka kwa Wakenya wote ambao waliingiliana nao. Kazi ya wajumbe hao ilifadhiliwa na Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Marekani (USAID).       

I. MATOKEO NA MAPENDEKEZO YA AWALI

Wajumbe  wanasisitiza kwamba hii ni taarifa ya awali na wala siyo ya mwisho kuhusu uchaguzi wa 2022 na inatoa matokeo ya awali na mapendekezo kulingana na muktadha mpana wa uchaguzi hasa; kipindi cha kabla ya uchaguzi na Siku ya Uchaguzi kupitia upigaji na kuhesabu kura. Ni muhimu kukumbuka kwamba, taratibu muhimu za kujumlisha na kutangaza matokeo bado zinaendelea; matokeo rasmi bado hayajatangazwa; na changamoto za uchaguzi kama zipo, bado hazijashuluhishwa.

Uchaguzi wa 2022 umefanyika dhidi ya chaguzi tatu za mfuatano zenye utata. Kutokana na ukomo wa mihula ya kikatiba, Wakenya watakuwa wakimchagua rais mpya kwa mara ya tatu tangu kuanzishwa upya kwa siasa za vyama vingi. Muktadha wa sasa wa kisiasa unaonyesha upatanisho wa ushirikiano kati ya vyama vikuu vya kisiasa na kuonyesha hali ya mabadiliko ya mazingira ya uchaguzi. Katika uchaguzi wa sasa, miungano iliegemezwa zaidi kwenye sera. Hata hivyo, siasa za utambulisho wa kikabila ni suala muhimu. Wagombea wakuu wawili wa urais ni Waziri Mkuu wa zamani Raila Odinga, kiongozi wa Azimio la Umoja  anayeungwa mkono na Rais Uhuru Kenyatta, mpinzani wake wa zamani wa kisiasa; na Naibu Rais wa sasa William Ruto, kiongozi wa muungano wa Kenya Kwanza na mshiriki  wa zamani wa Rais Kenyatta.

Uchaguzi wa 2022 bado haujakamilika. Kumekuwa na mchakato mzuri hasa katika baadhi ya vipengele vya uchaguzi kama vile; kipindi cha amani kabla ya uchaguzi, kuboreshwa kwa mchakato wa uteuzi wa wagombea na ongezeko la wagombea wanawake. Siku ya uchaguzi wapiga kura waliweza kupiga kura kwa wagombea waliowachagua kwa utaratibu wa kawaida na wa amani. Hata hivyo, Uchaguzi huu umekumbwa na changamoto kama vile; mabadiliko ya dakika za mwisho kuhusu taratibu za uchaguzi, usalama na wakati unaofaa wa uwasilishaji na utangazaji wa matokeo. Changamoto hizi zinaweza kupunguza uaminifu uliokuwepo hapo awali na kutishia imani katika mchakato wa uchaguzi. Katika saa na siku zijazo, tunahimiza pande zote kuzingatia sheria za Kenya kikamilifu na kuruhusu michakato ya uchaguzi kukamilika bila kuingiliwa.

Uchaguzi mkuu wa 2022 nchini Kenya umehusisha zaidi wagombea wa kike na katika kipindi cha kabla ya uchaguzi kulikuwa na amani tofauti na  miaka ya awali. Sheria ya vyama vya Siasa ilirekebishwa ili kuchangia michakato ya amani zaidi kwenye uteuzi wa wagombea, lakini sio wazi zaidi. Idadi ya wagombea wanawake pia iliongezeka. Vilevile, kwa mara ya kwanza, wagombea watatu wa naibu rais ni wa kike. Idadi ya wagombea wanawake wa naibu ugavana pia iliongezeka maradufu kutoka 30 mwaka wa 2017 hadi 62 mwaka wa 2022. Hata hivyo, sheria ya kutokuwa na zaidi ya theluthi mbili ya jinsia moja bado haijapitishwa. Ingawa mfumo wa kisheria wa Kenya unatoa msingi mzuri wa uchaguzi wa kuaminika, juhudi za kusasisha sheria na kanuni kwa kuzingatia kubatilishwa kwa uchaguzi wa uraisi mwaka 2017 na  Mahakama ya Juu hazijafaulu. Idara ya mahakama inaheshimiwa sana miongoni mwa Wakenya katika wigo wa kisiasa na kwa mashirika ya kiraia kwa kuwa na imani na uwezo wa kushughulikia mizozo inayohusiana na uchaguzi. Tume ya uchaguzi nchini Kenya, IEBC, ilichukua hatua muhimu kuimarisha mawasiliano kwa washikadau wakuu. Pia, iliingia katika mkataba wa makubaliano (MOU) na vyombo vikuu vya habari kwa ajili ya ujumlishaji huru wa matokeo ya uchaguzi. Kufuatia kura za mchujo za vigingi vingi, mazingira ya kampeni yalikuwa ya amani kiasi isipokuwa matukio machache ya ghasia. Licha ya vikwazo vya ufadhili, mashirika ya kiraia yalishiriki kikamilifu katika juhudi za kupunguza vurugu na kuleta amani, uangalizi wa uchaguzi na kufuatilia vurugu dhidi ya wanawake katika chaguzi. Muhimu zaidi, katika kipindi cha kabla ya uchaguzi, kulikuwa na uboreshaji mkubwa katika mazingira ya usalama ingawa wagombea wakuu wa urais walikataa kutia saini ahadi za amani kibinafsi

Wakati huo huo, masuala kadhaa ya wasiwasi yalizuka katika kipindi cha kabla ya uchaguzi ambayo yangeweza kudhoofisha uaminifu wa mchakato huo. Ingawa kuna zaidi ya wapigakura milioni 22 waliojiandikisha, idadi hii haikufikia matarajio. Isitoshe, usajili wa wapigakura vijana wenye umri wa miaka 18 hadi 35 imepungua  ikilinganishwa na mwaka wa 2013. Kutoridhika kwa vijana na kutokuwa na imani na uchaguzi kuliripotiwa kuwa changamoto kubwa kabla ya uchaguzi wa 2022. Hii inaonekana katika viwango vya chini vya usajili wa wapiga kura vijana haswa kwa wale ambao wametimiza miaka 18 tangu uchaguzi wa 2017. Tofauti na 2017, ripoti ya ukaguzi wa KPMG ya rejista ya wapiga kura ilicheleweshwa  na kutolewa kwa kiasi, hivyo basi kupunguza uwazi. Sheria ya fedha za kampeni bado haijatekelezwa na Mahakama ilikataa kurejesha vikomo vya matumizi. Matokeo yake ni kwamba gharama ya uchaguzi inasalia kuwa juu sana kwa wengi hasa wagombea wanawake. Wagombea wengi wa kike waliripoti vurugu ya matusi na vitendo vingine vya ukatili wa kisaikolojia kutoka kwa wapinzani; wanaume, wanawake na wafuasi wao. Jitihada chache za dhati zilifanywa kuongeza ushiriki wa watu wenye ulemavu (walemavu). Taarifa potofu zilizoenea katika mitandao ya kijamii zilikuwa kwa manufaa ya pande zote mbili kuu za kisiasa.

Mkesha wa uchaguzi kulikuwa na mkanganyiko mkubwa kuhusu taratibu za uchaguzi kufuatia maamuzi ya dakika za mwisho kuhusiana na matumizi ya rejista ya wapiga kura, taratibu za kura zilizoharibika na uwasilishaji wa matokeo rasmi ya kura za urais kwenye vituo vya kupigia kura (fomu 34A). Hili lilidhoofisha juhudi za IEBC za kuwafunza wafanyikazi wa vituo cha kupigia kura na kuhakikisha utumizi thabiti wa taratibu za upigaji kura na kuhesabu kura. Aidha, hitilafu za uchapishaji wa karatasi za kura zilisababisha chaguzi nne kulazimika kucheleweshwa katika dakika za mwisho zikiwemo za ugavana katika kaunti za Kakamega na Mombasa.

Siku ya uchaguzi yenyewe, kulikuwa na amani. Vituo vingi vya kupigia kura vilifunguliwa kwa wakati na nyenzo zote zinazohusiana na uchaguzi zilikuwepo. Wapiga kura, wakiwemo wanawake, walisubiri kwa utulivu katika foleni ndefu. Kulikuwa na visa vichache vya Mfumo wa Kusimamia Uchaguzi wa Kenya (KIEMS) kutofanya  kazi. Seti za KIEMS mara kwa mara zilichukua majaribio kadhaa kuthibitisha wapigakura lakini hazikusababisha watu wanaostahiki kutoruhusiwa kupiga kura. Maafisa wa upigaji kura walifanya kila juhudi kuhakikisha watu wote waliohitimu waliweza kupiga kura. Vikosi vya usalama vilifanya kazi kwa weledi na havikuingilia mchakato huo. Mkanganyiko uliendelea kuhusu jukumu la nakala zilizochapishwa za rejista ya wapigakura. Kwa ujumla rejista zilizokuwepo hazikutumika kwa utambulisho wa mpigakura mwenyewe au kurekodi kwa mikono ni nani aliyepiga kura. Karatasi sita za kupiga kura zilisababisha mkanganyiko na wakati fulani, kura iliwekwa kwenye sanduku lisilo sahihi na kukataliwa baadaye. Kuhesabu kura kulifanyika kwa uwazi mbele ya maajenti wa vyama na mara nyingi waangalizi wa wananchi. Ijapokuwa  maajenti wa vyama vinavyoshiriki uchaguzi wa urais walipewa nakala ya fomu rasmi ya matokeo ya 34A, mara nyingi nakala haikubandikwa wakati wa kuhesabu kura ili umma ione, tofauti na chaguzi za awali.

Kabla ya Siku ya Uchaguzi, IEBC ilifanya majaribio mawili hata hivyo, mazoezi yote yalikuwa na upungufu. Hofu hasa ni vituo 1,000 vya kupigia kura visivyo na mawasiliano ya simu ya rununu ya 3G vilivyohitaji  teknolojia ya satelaiti kwa upitishaji wa kielektroniki. Ili kuimarisha uwazi, IEBC ilianzisha tovuti yenye picha zilizochanganuliwa za fomu za matokeo ya uraisi,fomu 34A. Isitoshe, vyombo vya habari na vyama vya siasa vimendesha ujulishajizaowa sambamba na IEBC. Ingawa haya yana uwezo wa kuimarisha uwazi, yanaweza pia kupotosha na kuleta mkanganyiko ikiwa hayatafanywa kitaalamu. Muhimu zaidi ni kwamba, waangalizi wa raia wamejumlisha kura sawia (PVT) kwa uchaguzi wa urais kwa niaba ya Wakenya wote na kwa nia  ya kudumisha uadilifu wa uchaguzi. PVTs hutoa habari inayowakilisha ukweli kuhusu upigaji kura na kuhesabu kura pamoja na uthibitishaji wa wakati halisi wa matokeo rasmi kama yalivyotangazwa na IEBC.

Wajumbe wa IRI/NDI wanasisitiza kwamba hii ni kauli ya awali na inajumuisha matokeo ya awali na mapendekezo. Wakati mchakato wa kujumlisha ukiendelea, wajumbe wa pamoja wa NDI/IRI wametoa wito kwa vyama vyote, wagombea na wafuasi wao kuzingatia ahadi walizotoa kwa uchaguzi wa amani na kukataa vurugu. Mizozo ikitokea, tunatoa wito kwa wahusika wote kuisuluhisha  kwa amani na kupitia njia zinazofaa za kiutaratibu na kisheria.

Kufuatia maswala haya, IRI na NDI wanatoa mapendekezo  yafuatayo ambayo yanaweza kuchukuliwa sasa ili kuongeza imani katika ujumlishaji na utangazaji wa matokeo na pia kuchangia  amani.

Kwa IEBC

Kwa Vyama vya Siasa na Wagombea

Waelekeze wafuasi hadharani kujiepusha na vitendo vyovyote vya vurugu wakati na baada ya kujumlisha na kutangaza matokeo.

Kwa Mahakama

Kwa Serikali

Kwa Vyombo vya Usalama

Kwa Asasi za Kiraia, Viongozi wa Dini na Vyombo vya Habari

Baada ya mchakato wa uchaguzi kukamilika, yafaa  kuwe na mpito wa mamlaka kwa amani na kwa wakati bila kujali matokeo. Changamoto zinazokabili uchaguzi wa Kenya si za kipekee , zinaathiri demokrasia changa na kongwe kote ulimwenguni. Kenya ni mwanga wa matumaini wakati huu muhimu ambapo demokrasia inakabiliwa na tishio kikanda na kimataifa. Kenya ina fursa sio tu kusonga mbele dhidi ya chaguzi zake za zamani, lakini pia kuwa kielelezo muhimu kwa Afrika na demokrasia zote ulimwenguni.

Baada ya uchaguzi wa 2022, tunatumai na kutarajia kwamba, Wakenya wote watafanya kazi pamoja ili kuhakikisha demokrasia ya Kenya inaboresha maisha ya raia wake wote hasa jamii zilizotengwa ikiwa ni pamoja na wanawake, vijana, na watu wenye ulemavu.

Wajumbe wa pamoja wa NDI/IRI wataendelea kufuatilia maendeleo ya uchaguzi ikiwa ni pamoja na mchakato wa kujumlisha, kusuluhisha mizozo, kutangaza matokeo rasmi na kuapishwa kwa maafisa wapya waliochaguliwa na inaweza kutoa taarifa na ufafanuzi zaidi kama inavyohitajika. Baada ya hitimisho la Uchaguzi wa Agosti 9, 2022, IRI na NDI zitatoa ripoti ya kina inayoeleza matokeo ya mwisho na mapendekezo.

I. MATOKEO YAKINA

Uchaguzi wa 2022 unafanyika wakati ambapo matokeo ya urais ya chaguzi tatu zilizopita yalipingwa. Uchaguzi wa mwisho wa urais ambao haukupingwa  ulikuwa wa mwaka wa 2002. Mwaka 2007, wasiwasi mkubwa kuhusu  mchakato wa kujumlisha kura na usahihi wa matokeo ya urais ulizua ghasia zilizoenea baada ya uchaguzi. Baadaye, mfumo wa kisheria wa Kenya wa uchaguzi ulifanyiwa mageuzi makubwa na kusababisha kuwepo kwa; Katiba mpya, Sheria ya Uchaguzi na sheria na kanuni zinazohusiana. Uchaguzi wa urais mwaka wa 2013, uliendeshwa chini ya mfumo mpya wa kisheria, uliomzuia mgombea aliyeshinda kuepuka rudio la pili kwa zaidi ya asilimia 50 ya kura. Matokeo hayo yalipingwa katika mahakama, ambayo ilidumisha matokeo huku ikikubali masuala ya mchakato huo. Ingawa kiwango cha ushindi katika uchaguzi wa urais wa 2017 kilikuwa kikubwa zaidi kuliko mwaka wa 2013, matokeo yalipingwa tena. Safari hii mahakama ilibatilisha matokeo hayo kutokana na tume ya uchaguzi kushindwa kufuata matakwa ya kisheria badala  ya ushahidi kuwepo kuwa matokeo yalikuwa yamefanyiwa ukarabati. Upinzani hata hivyo, ulisusia marudio ya uchaguzi yaliyofuata na kusababisha upigaji kura kutowezekana katika maeneo mengi na idadi ya waliojitokeza kuwa chini ya asilimia 40 (kutoka karibu asilimia 80 ). Ni kutokana na historia  hii ambapo uchaguzi wa 2022 unefanyika.

Mfumo wa Kisheria

Vipengele muhimu vya mfumo wa kisheria vya uchaguzi ni pamoja na Katiba ya Kenya, Sheria ya Uchaguzi ya 2011 na kanuni zinazohusiana, Sheria ya Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka ya 2011, Sheria ya Vyama vya Siasa ya 2011, na Sheria ya Hatia za Uchaguzi ya 2016. Mfumo wa kisheria ulibadilishwa kwa kiasi kikubwa kukabiliana na uchaguzi wa 2007 na ghasia zilizofuata baada ya uchaguzi.

Marekebisho ya hivi majuzi ya mswada wa vyama vya kisiasa  yalipitishwa kuwa sheria mwaka wa 2022 licha ya upinzani mkali kutoka kwa Ruto kuhusu mabadiliko yaliyoletwa kama vile tofauti kati ya vyama na miungano na vile vile sharti jipya la vyama kuhitajika kuchapisha na kuwasilisha mchakato wao wa uteuzi kwa Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa (ORPP). Ingawa baadhi walibainisha kuwa marekebisho hayo yalichangia mchakato wa uteuzi wa amani zaidi, mbinu zisizo za moja kwa moja za uteuzi pia ziliibua maswali ya uwazi na ushirikishi. Hata hivyo, marekebisho ya Sheria ya Uchaguzi ambayo yalitaka kushughulikia masuala yaliyotolewa na uamuzi wa Mahakama ya Juu baada ya uchaguzi wa 2017 yalipitishwa na Bunge la Kitaifa lakini hayakufanyiwa kazi na Seneti.

Mahakama

Idara ya mahakama ilivuta imani ya watu na ilifanya kazi kwa bidii ili kuimarisha uwezo wake wa kushughulikia ukiukaji wa sheria na malalamiko yanayohusiana na uchaguzi. Majaji, mahakimu, na wafanyakazi wa mahakama walipata mafunzo kuhusu vipengele vya mchakato wa uchaguzi ikiwa ni pamoja na; taratibu za utumaji matokeo na teknolojia zinazohusiana. Aidha, kitabu cha benchi ambacho ni muunganisho wa kesi zote zinazohusiana na uchaguzi na nyenzo za mahakama kilitayarishwa kwa ajili ya wajumbe wote wa mahakama inayoshughulikia malalamiko ya uchaguzi. Mfumo wa kielektroniki wa kufungua jalada pia ulipatikana na uwezo wa kusikiliza maombi pia ulianzishwa. Hata hivyo, hii itategemea mienendo ya kesi.

Utawala wa Uchaguzi

Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka: IEBC ni Tume huru kikatiba inayojumuisha Mwenyekiti na makamishna sita ambao wanatambuliwa na jopo la uteuzi lililoteuliwa na Rais, kuidhinishwa na Bunge la Kitaifa, na kuteuliwa na Rais. Mwenyekiti na makamishna wawili waliteuliwa mwishoni mwa Januari 2017 huku makamishna wanne wakihudumu kama kaimu hadi walipoteuliwa Septemba 2021. Uchaguzi nchini Kenya unasimamiwa na usimamizi wa uchaguzi wa ngazi nne unaojumuisha Tume na Ofisi Kuu mjini Nairobi,Ofisi 47 za kaunti , Ofisi 290 za maeneobunge, na vituo 46,229 vya kupigia kura.

Usajili wa Wapigakura: IEBC ilifunga usajili wa wapigakura mnamo Mei 4 licha ya Sheria ya Uchaguzi kuagiza  usajili kuendelea hadi siku 60 kabla ya uchaguzi. Baada ya hapo, wapigakura waliweza kuthibitisha hali yao ya kujiandikisha kwa kujitokeza kibinafsi, mtandaoni, au kupitia SMS kwa muda wa siku 30 hadi Juni 2. Orodha ya mwisho ya wapigakura ilijumuisha wapigakura 22,120,458 (takriban asilimia 85 ya wapigakura wanaostahiki), wakiwemo wapigakura 10,443 nje ya nchi na 7,483 kwenye magereza . Idadi  ya wapiga kura waliojiandikisha iliongezeka kwa asilimia 12.79, ikilinganishwa na 2017. Hata hivyo,  kwa jumla  wapigakura wapya waliosajiliwa walikuwa 2,509,035, idadi ambayo haikufikia lengo la IEBC la milioni sita.

IEBC iliidhinisha KPMG kufanya ukaguzi huru wa rejista ya wapiga kura. Kama sehemu ya ukaguzi, KPMG ilitoa mapendekezo kuhusu masuala kama vile kuimarisha udhibiti wa utumaji maombi, hifadhi data na miundombinu ili kuhakikisha usalama wa rejista ya wapigakura. Ukaguzi huo pia ulipata vighairi kadhaa ambavyo IEBC ilishughulikia, kama vile visa vya wapiga kura walioaga dunia na pasipoti batili au nambari za utambulisho. Kufuatia kukamilika kwa ukaguzi huo, mnamo Juni 16, IEBC ilidokeza kuwa nakala ya ripoti hiyo iliwasilishwa kwa Bunge la Kitaifa na Seneti kwa mujibu wa Sheria ya Uchaguzi. Wadau waliendelea kutoa wito kwa ripoti ya mwisho ya ukaguzi wa KPMG kushirikiwa na umma. Mnamo Agosti 2, IEBC ilichapisha sehemu ya ripoti ya ukaguzi pamoja na muktadha wa utekelezaji wa mapendekezo ya ukaguzi huo.

Uteuzi wa Vyama na Usajili wa Wagombea: Mnamo Aprili 2022, vyama vya siasa vilifanya uteuzi wao ili kuchagua wagombea wao kwa nafasi sita za kuchaguliwa. Chini ya marekebisho ya 2022 ya Sheria ya Vyama vya Kisiasa (2011), vyama vinaruhusiwa kuteua wagombea moja kwa moja kupitia idhini ya wote ya uanachama wao au kuwateua kwa njia isiyo ya moja kwa moja kupitia maafikiano, kura za maoni za ndani, wajumbe au mbinu zingine. Mchakato huo mara nyingi haukuwa wazi na uliharibiwa na chaguzi za upendeleo juu ya michakato ya ushindani ambao mara nyingi uliwatenga wenye nia ya kugombea hasa vijana na zaidi wanawake wachanga. Kutokana na hali hiyo, wagombea wengi walichagua kugombea kama wagombea huru na IEBC ilipokea maombi ya usajili kutoka kwa wagombea huru zaidi ya 7,000, lakini ni 4,526 pekee walioidhinishwa, ikiwa ni asilimia 28 ya wagombea wote.

Muda wa uandikishaji wa wagombea ulianza Mei 29 na kumalizika Juni 10. Jumla ya wagombea 16,100 waliruhusiwa kugombea katika uchaguzi wa 2022, kati yao 11,574 waliwakilisha vyama vya siasa (asilimia 72) huku 4,526 (asilimia 28) wakiwa wagombea huru. Hii inajumuisha wagombea wanne wa urais; 266 kwa ugavana; 341 kwa Seneti; 360 kwa mwakilishi wa wanawake; 2,132 kwa wajumbe wa Bunge; na 12,997 kwa wanachama wa Bunge la Kaunti.

Kama sehemu ya mchakato wa usajili, IEBC iliwasilisha orodha ya wawaniaji 21,865 kwa Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) ili kuzingatia kufuata mahitaji ya uongozi na uadilifu kwa mujibu wa Sura ya sita ya Katiba. Kati ya waliowasilishwa, wawaniaji 241 waliangaziwa kwa masuala ya uadilifu kama vile ufisadi au utumizi mbaya wa afisi huku ikipendekezwa kuwa IEBC izingatie maswala haya kabla ya kuwaondoa wagombea. Licha ya matokeo ya EACC, IEBC haikufutilia mbali idadi kubwa ya wawaniaji hao, ikitaja vipengee vya kikatiba vya kudhaniwa kuwa hawana hatia hadi ithibitishwe na hatia miongoni mwa mengine. Tume ya IEBC na EACC ziliendelea kutokubaliana kuhusu mamlaka na wajibu wao kuhusu kuidhinishwa kwa wagombea na masuala ya uadilifu. Aidha, washikadau walionyesha kufadhaika kuhusu upungufu katika utumiaji wa mahitaji hayo pamoja na wasiwasi kwamba  matokeo yake yangekuwa wagombea wenye masuala ya uadilifu kuchaguliwa.

Teknolojia ya Uchaguzi: IEBC ilianzisha teknolojia ya uthibitishaji wa wapigakura kwa njia ya kibayometriki na utumaji matokeo ya kielektroniki inayojulikana kwa pamoja kama Mfumo wa Kusimamia Uchaguzi wa Kenya (KIEMS). Kando na utambulisho wa kibayometriki, sheria inaitaka IEBC kuweka mbinu ya ziada ya kuwatambua wapigakura siku ya uchaguzi. IEBC iliamua kwamba mbinu za msingi na za ziada za utambulisho zingetegemea rejista ya wapigakura  ya kidijitali iliyopakiwa kwenye kadi salama ya kumbukumbu ya kidijitali katika kila kifurushi cha KIEMS badala ya kutumia nakala halisi ya rejista kama mbinu ya ziada. Iwapo mpiga kura hakutambuliwa kibayometriki, walitambuliwa kwa herufi na nambari kwa kuweka kitambulisho chake au nambari ya pasipoti kwenye kifaa cha KIEMS. Kila wadi ilikuwa na vifaa sita vya kuhifadhia nafasi ya seti iliyofeli katika kituo cha kupigia kura. Kulingana na IEBC, uamuzi wao wa kutotumia rejista ngumu ulikuwa juhudi za kuzuia hitilafu za upigaji kura. IEBC baadaye ilifafanua kwamba nakala halisi iliyofungwa ya rejista ingepatikana katika kila kituo cha kupigia kura ili kutumika kama suluhu ya mwisho. Hata hivyo, washikadau walielezea wasiwasi wao kuhusu uamuzi wa IEBC. Aidha, mashirika kadhaa ya kijamii (CSOs) yaliwasilisha ombi katika Mahakama Kuu kutaka kulazimisha IEBC kutumia sajili hiyo halisi.

Mfumo wa Usambazaji wa Matokeo: Kwa mujibu wa matakwa ya kisheria ya kujaribu mfumo wa uwasilishaji matokeo  siku 60 kabla ya uchaguzi kwa mujibu wa kifungu cha 44 cha Sheria ya Uchaguzi,, IBEC ilifanya uigaji wa mchakato wa utumaji matokeo Juni 9. Wakati huo huo, IEBC ilitangaza vipengele vilivyoimarishwa vya usalama, kama vile Mitandao ya Kibinafsi (VPN), ngome na misimbo wa ufikiaji wa usalama ili kuzuia visa vya udukuzi na uundaji wa tovuti ya umma ya kuchapisha skani za fomu za matokeo fomu 34A ambazo zilikuwa zikipitishwa kutoka vituo vya kupigia kura hadi eneo bunge na vituo vya  kitaifa vya kuhesabia kura. Uigaji huo ulihusisha sampuli ya vituo 2,900 vya kupigia kura au vituo viwili vya kupigia kura katika kila wadi kati ya wadi 1,450. Hata hivyo, kufikia wakati zoezi la kuiga lilipokamilika, baada ya takriban saa mbili na nusu,  ni chini ya nusu ya matokeo ya vituo 2,900 vya kupigia kura yalikuwa yamepokelewa. Wakati na baada ya uigaji, wasiwasi ulionyeshwa kuhusu uwasilishaji polepole wa fomu, muundo wa tovuti ya umma, njia ambayo matokeo yangehesabiwa katika kituo cha kitaifa cha kuhesabia, usalama wa mchakato wa uwasilishaji na masuala mengine. Mnamo Julai 19, IEBC ilifanya zoezi la pili la kuiga lililohusisha vituo 580 pekee kutokana na utendakazi na utayarishaji wa vifaa vya KIEMS Nairobi. Zaidi ya hayo, IEBC iliwasilisha toleo jipya la tovuti ya umma, ambalo lilikuwa limejumuisha maoni kutoka kwa washikadau kufuatia uigaji wa kwanza.

Katika kipindi chote cha kabla ya uchaguzi, mashirika ya kiraia, vyama vya kisiasa na vyombo vya habari mara kwa mara vilieleza kuchoshwa na kutokuwepo kwa mawasiliano ya mara kwa mara kutoka kwa IEBC na mwitikio wake wa polepole kwa maombi ya habari, jambo ambalo lilizua wasiwasi kuhusu  hali ya utayari na uwazi wa tume hiyo kusimamia kura  zenye ubora. Changamoto za mawasiliano pia zilitajwa kuwa kikwazo cha kusimamia vyema matarajio ya umma na kusababisha taarifa zinazokinzana kuhusu mchakato wa usimamizi wa matokeo. Kwa upande wake, IEBC iliripoti kuongezeka kwa propaganda, madai ya uongo na majaribio ya kuwalenga wafanyikazi wa IEBC. Kutokana na hali hiyo, IEBC ilimtaka Mkurugenzi wa Uchunguzi wa Jinai (DCI) kuchunguza propaganda hizo pamoja na kuimarisha usalama wa maafisa wa uchaguzi kote nchini.

Vyama vya Siasa na Kampeni

Mazingira ya Kampeni: Kipindi cha kampeni kilianza rasmi Mei 29 na kumalizika saa 48 kabla ya uchaguzi wa Agosti 9. Uhuru wa kukusanyika, kujieleza na kujumuika uliheshimiwa kwa mapana licha ya visa vya ghasia vilivyorekodiwa katika angalau kaunti 27. Kufikia Agosti 6, mashambulizi ya kimwili dhidi ya wagombea na wafuasi wao yalirekodiwa Nairobi (21), Bungoma (17), Busia (10), Uasin Gishu (7), Homa Bay (5), Migori (5), Kakamega (4) , kaunti za Mombasa (4), Machakos (3), na Siaya (3). Kulikuwa na uchache wa  vyama vingi vya kisiasa katika ngome za vyama ambapo wagombea waliojiunga na muungano pinzani mara nyingi waliendesha shughuli zao katika nafasi ndogo za kisiasa na fursa chache za kufanya kampeni kimasomaso.

Azimio la Umoja (One Kenya Coalition) na Kenya Kwanza ziliweka ratiba kamili za kampeni na kuandaa mikutano mikubwa ya kuwania urais katika kaunti zote 47. Wakati miungano yote miwili ilianzisha mashirika ya kampeni ya kieneo ili kuratibu shughuli za wagombeaji wao wa urais, wanachama binafsi wa chama walikuwa na jukumu la kuunga mkono wagombea wao kutoka nafasi ya ugavana hadi mjumbe wa bunge la kaunti. Makubaliano ya kabla ya uchaguzi yanayoruhusu usajili wa mgombea mmoja wa muungano yalitekelezwa katika maeneo machache ya uchaguzi. Hata hivyo, mara nyingi, viongozi wa Azimio na Kenya Kwanza hawakuweza kuwashawishi wagombea kutoka vyama vidogo kujiondoa na kuuunga mkono vyama vyenye nguvu zaidi. Hata hivyo, wagombea hao  walighairi mipango  ya vyama hivyo mingi ya ukandaamizaji kufuatia kukamilishwa kwa orodha ya wagombea wa IEBC. Azimio la Umoja  na Kenya Kwanza walikumbwa na migawanyiko ya ndani kwa ndani na kutoelewana katika kaunti nyingi ambapo wanachama wa vyama vya muungano walipanga wagombea wengi.

Ingawa wagombea urais wote wawili walijikita zaidi katika masuala ya ubinafsi wa mtu na ukosoaji wa IEBC, polisi na taasisi nyinginezo, pia walijadili vipengele muhimu vilivyojumuishwa kwenye manifesto zao. Ruto alielekeza kampeni yake katika ujumbe wa ‘hustler dhidi ya  dynasty kuimarisha mfumo wa “bottom-up”, ambao uliwavutia Vijana wengi kote nchini.. Odinga aliahidi kuimarisha sekta ya viwanda nchini Kenya, mfumo  wa serikali ya ugatuzi, na kupambana na ufisadi. Cha mno ni kuwa, kambi zote mbili ziliangazia masuala ya usawa wa kijinsia na ushirikishi, hasa katika mwezi wa kwanza wa kipindi cha kampeni.

Licha ya  Odinga kujiondoa katika mojawapo ya midahalo miwili ya urais, upeperushaji wa midahalo mingi ya wagombea ulisaidia kueleweka kwa kuwepo kwa mfumo wa vyama vingi vya kisiasa nchini Kenya na kuelimisha  wapiga kura. Kando na mijadala miwili ya urais na naibu wa rais, kulikuwepo na  mijadala ya Ugavanakatika angalau kaunti 29 iliyotangazwa moja kwa moja kwenye mitandao ya matangazo ya idhaa za  kiasili  na  mitandao ya kijamii. Mijadala mingi ya kuwatambulisha wagombea wa nyadhifa nyingine nne za kuchaguliwa pia iliendeshwa.[1]

Kutokana na kutotekelezwa kwa Sheria ya Ufadhili wa Kampeni za Uchaguzi (2013), Azimio la Umoja na Kenya Kwanza walitumia kiasi kikubwa cha fedha kuhamasisha wapigakura, bila kubanwa na kanuni za michango na matumizi ya hazina. Ununuzi wa kura umesalia kuenea nchini Kenya na visa mahususi vya usambazaji wa pesa au vyakula viliripotiwa kwa Ujumbe katika  kaunti za Nairobi, Nakuru, na Kisumu.[2] 

Malalamiko yaliibuka kutoka  pande zote mbili kuhusu madai juu ya matumizi mabaya ya rasilimali za serikali. Wakati wote wa kampeni, Kenya Kwanza iliishutumu Azimio kwa ‘state capture’ na kuelezea wasiwasi wake kuhusu kuhusika kwa makatibu wakuu wa baraza la mawaziri na makamishna wa kaunti katika shughuli za kisiasa, pamoja na kuingilia kati kwa Rais Uhuru Kenyatta katika mchakato wa uchaguzi[3] Kadhalika mnamo Juni 20, Azimio iliiandikia  IEBC ikidai kuwa naibu rais alikuwa akitumia pesa za afisi yake za ukarimu na makazi rasmi kufadhili na kuandaa mikusanyiko ya kisiasa ya Kenya Kwanza. Timu ya kampeni ya Odinga pia ilidai kuwa ofisi ya Ruto ilikuwa ikiajiri watumishi wa umma kueneza habari potofu kwenye vyombo vya habari na mitandao ya kijamii.

Usalama wa Uchaguzi

Kufuatia kura za mchujo ya vigingi vingi, mazingira ya kampeni yalikuwa ya amani kiasi bali na visa vichache vya vurugu. Uharibifu, uondoaji au uchakachuaji wa nyenzo za kampeni ulijumuisha wingi wa hatia za uchaguzi. Mashambulizi ya kimwili na mapigano kati ya wafuasi wa wapinzani, vijana wa kukodiwa na wagombeaji walengwa yalirekodiwa katika kaunti 27 na angalau watu wawili waliuawa Nairobi na Bungoma. Hali ya taharuki iliongezeka katika kaunti za Nairobi, Uasin Gishu, Siaya na Kisii.

Tangu 2017, huduma  za  usalama wa uchaguzi zimetolewa kupitia Mpango wa Maandalizi ya Usalama wa Uchaguzi (ESAP), mfumo wa mashirika mengi unao ongozwa na IEBC wakishirikiana na wahudumu kutoka ajenti nyingi. Kutokana na kutofautiana kati ya IEBC na Huduma ya Kitaifa ya Polisi (NPS), IEBC ilifutilia mbali mafunzo ya ESAP kuhusu usimamizi wa usalama wa uchaguzi mwishoni mwa Mei, miezi mitatu nyuma ya mpango wao wa awali. Wadau hao walielezea changamoto za ushirikiano kati ya taasisi hizo mbili katika ngazi ya kitaifa na kuonya dhidi ya uwekaji siasa wa migawanyiko yao. Jambo njema ni kwamba , NPS ilitunga miongozo ya mafunzo pamoja na mitaala ya mafunzo kwa ushirikiano na Mamlaka Huru ya Kusimamia Polisi (IPOA) na mashirika ya kimataifa na ya kitaifa ya haki za binadamu. Mafunzo kuhusu wajibu wa uchaguzi, ikiwa ni pamoja na udhibiti wa umati, haki za binadamu, unyanyasaji wa kijinsia na kiuana (SGBV) na uwajibikaji wa polisi, yalitolewa kutoka kanda hadi kaunti ndogo. Licha ya Inspekta Jenerali wa Polisi (IG) kutangaza Julai 22 kwamba maafisa wote wa polisi wamefunzwa, washikadau walionyesha mashaka yao makubwa juu ya uwezo wao wa kutoa mafunzo kwa maafisa wa ngazi za chini kwa wakati ufaao na kuelezea wasiwasi wao kwamba mpango wa kutumiwa haukutolewa kwa umma.

Kwa lengo la kuzuia mizozo iliyokuwepo awali na kuzuia ghasia za uchaguzi, NPS ilipeleka vitengo vya ziada katika maeneo yenye mizozo na kisha ikatekeleza amri za kutotoka nje huko Marsabit na sehemu za Baringo, Pokot Magharibi na Elgeyo Marakwet, kuitisha mikutano kati pande zinazozozana  ya usalama ya dharura, na kushiriki mara kwa mara katika mikutano ya sekta mbalimbali kuhusu maandalizi ya uchaguzi. Washikadau walikaribisha matayarisho ya polisi kushauriana na makundi ya kiraia na uwazi wao katika upashanaji habari ambao unachangia katika kuziba pengo la mawasiliano na mashirika ya nyanjani, kushughulikia ukosefu wa uaminifu, na kuimarisha mifumo ya mwitikio. Hata hivyo, ripoti za ushirikiano kati ya NPS na tawala za kaunti katika kaunti za Kisumu, Uasin Gishu, na Siaya huenda zilidhoofisha mipango hii.

Utekelezaji wa Kanuni za Maadili za Sheria ya Uchaguzi ulikuwa mdogo sana. Washikadau mbalimbali waliendeleza uchaguzi kwa amani lakini wagombea wachache walitaka kuheshimiwa kwa kanuni za maadili isipokuwa wakati wao au wafuasi wao walishambuliwa. Vyombo vya habari pia viliripoti mara kwa mara kwamba makosa mbalimbali ya uchaguzi yalikuwa yakichunguzwa na DCI..Hata hivyo ni machache yamehitimishwa hadi sasa.

Juhudi za Amani na kupunguza Vurugu: Kama sehemu ya mwelekeo wa Uchaguzi Bila Noma, kuelekeza uchaguzi wa amani, mpango wa Tume ya Kitaifa ya Uwiano na Utangamano (NCIC), mashirika ya serikali na wahusika wa amani wasio wa serikali walianzisha mfululizo wa shughuli za amani chini ya jukwaa la UWIANO[4] na kampeni ya #LetPeaceWin (Wacha Amani Ishinde) iliyozinduliwa Juni 18. Ingawa utendakazi wa mkakati wa jumla ulisalia kuwa fiche, mashirika yalilenga hasa kaunti zenye mizozo zilizotambuliwa kupitia uchunguzi wa ramani ya maeneo yenye dalili za kuwa na mizozo mikali uliotolewa mwishoni mwa Mei na NCIC. Ramani ya maeneo yenye uwezo wa kuwa na mizozo mikali ilionyesha kaunti 16 ambazo zilikuwa katika hatari zaidi ya ghasia za uchaguzi huku Nairobi, Nakuru, Kericho, Kisumu, Uasin Gishu, na Mombasa, zikiwa miongoni mwa sita kuu.. Shughuli za amani zilijumuisha misafara ya amani, kukimbia na kutembea kwa amani, vituo vya masuala ibuka, na jukwaa za mashauriano na vyombo vya habari, bodaboda, vyama vya siasa, vikundi vya kiraia(CSO), vikundi vya kidini (FBO), wanawake na watu wenye ulemavu. Juhudi zinazolenga vijana na kuzuia ukatili dhidi yao pia zilitekelezwa.

Juhudi za kutafuta amani za NCIC zilitambuliwa kuwa zenye manufaa zaidi kuliko za chaguzi zilizopita. Hata hivyo, washikadau wote walilalamika kwamba Tume haikuwa na uwezo wa kuwafanya watoaji wa hotuba zenye madhara kuwajibika. Wengine pia walitilia shaka juu ya uhuru wake. Zaidi ya hayo, ilikuwa vigumu kuelewa jinsiTume ilivyoweza kufuatilia maelfu ya ahadi ambazo zilidaiwa kutiwa saini.

Unyanyasaji dhidi ya wanawake katika chaguzi: Kulingana na washikadau, unyanyasaji wa kiuana (GBV) na  unyanyasaji wa kijinsia (SGBV) umeenea na ulitekelezwa na na vijana waliokodiwa  na wagombea wanaume na wanawake, wafuasi na wakazi. Ujumbe  ulikusanya ripoti za wagombea wanawake kushambuliwa kimwili katika kaunti za Bungoma, Kirinyaga na Mombasa. Katika vikao mbalimbali vya wagombea wanawake, wanawake pia waliripoti kuwa walikumbwa na vitisho, matusi, na propaganda kuhusu maadili yao ya ngono, hali ya ndoa, na umri. Licha ya mfumo thabiti wa kisheria na umakini mkubwa wa unyanyasaji wa kijinsia, Shirika  la Wanasheria Wanawake la Kenya (FIDA-Kenya) lilitambua kesi 656 za dhuluma za kijinsia kuhusiana na uchaguzi kati ya mwanzo wa kura ya mchujo na mwishoni mwa Juni 2022. Kifungu cha 10 cha Sheria ya Hatia za Uchaguzi kinakataza matumizi au tishio la kutumia nguvu na unyanyasaji, ikiwa ni pamoja na unyanyasaji wa kijinsia, lakini linaacha kutajwa kwa GBV na SGBV, ambayo ingeruhusu mahakama kushughulikia hatia kwa haraka zaidi. Sheria ya Hatia za Kujamiiana ya 2006 inashughulikia aina nyingi za unyanyasaji wa kijinsia, ikiwa ni pamoja na ubakaji na unyanyasaji wa kijinsia, lakini inashindwa kushughulikia aina za kisasa za unyanyasaji wa kingono mtandaoni, ambao unawakilisha zaidi ya asilimia 30 ya kesi zilizoripotiwa na FIDA-Kenya.

Ujumuishi: Wanawake, Vijana, na Watu Wenye Ulemavu

Wakati Katiba ya Kenya ya 2010 ilipoidhinishwa, ilisifiwa kama mojawapo ya maendeleo zaidi duniani kwa haki za wanawake na walio wachache. Ingawa inatoa mfumo wa mchakato shirikishi wa kisiasa, vikwazo vya kuongeza uwakilishi wa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu katika maisha ya kisiasa vinaendelea kuwepo.

Ushiriki wa Wanawake: Wanawake wanawakilisha asilimia 49.12 ya wapiga kura waliojiandikisha, huku wanaume wakiwakilisha asilimia 50.88, kuonyesha kuwa  idadi ya wanawake bado ni ndogo katika rejista la wapiga kura. Katiba ya mwaka wa 2010 inabainisha  kwamba si zaidi ya theluthi mbili ya jinsia moja inaweza kuchukua fursa katika mashirika ya umma yaliyochaguliwa. Hata hivyo, zaidi ya miaka 10 baadaye, serikali bado haijatunga sheria ya kutekeleza kikamilifu matakwa haya ya kikatiba. Ni jambo la kuvutia kuwa wanawake wengi zaidi waligombea viti mwaka 2022 kuliko mwaka 2017. kwa idadi kamili na kama sehemu ya jumla ya idadi ya wagombea. Kulingana na IEBC, kati ya wagombea 16,100 walioidhinishwa katika uchaguzi wa 2022, wanawake wanawakilisha asilimia 12.18 au wagombea 1,962. Wagombea watatu kati ya wanne wa urais walimteua mwanamke kama mgombea mwenza na vyama kadhaa vya kisiasa viliteua wanawake kama katibu mkuu au mkurugenzi mtendaji. Kwa mara ya kwanza, ORPP ilitekeleza sheria ya kutozidi theluthi mbili ya jinsia moja  kwenye orodha ya wanachama .

Licha ya haya, wagombea wanawake nchini Kenya wanaendelea kukabiliwa na vikwazo vya kitamaduni na kiuchumi katika ushiriki wa kisiasa. Wagombea wengi wanawake wanakosa uwezo wa kukusanya rasilimali kuendeleza kampeni zao katika kipindi chote cha uchaguzi, wanasalia kutengwa na mitandao ya biashara na hawashiriki katika hafla zisizo rasmi za kukusanya pesa ambazo kwa kawaida hufanyika saa za jioni. Katika kipindi cha uchaguzi wa 2022, wagombea wanawake walinyanyaswa mtandaoni na kwenye kampeni, jambo ambalo huenda lilitatiza uwezo wao wa kutembea kwa uhuru na kutangamana na wapiga kura. Wanawake wengi wagombea  pia walikabiliwa na unyanyasaji wa maneno na vitendo vingine vya ukatili wa kisaikolojia kutoka kwa wapinzani wa kiume na wa kike na wafuasi wao, ambao mara nyingi walikosoa maumbile yao ya kimwili au hali ya kuwa kwenye ndoa.[5]

Ushiriki wa Vijana: Kutoridhika kwa vijana na kutojali kuhusu upigaji wa kura kuliripotiwa kuwa changamoto kubwa kabla ya uchaguzi wa 2022. Hii ilionekana katika viwango vya chini vya usajili wa wapigakura vijana, haswa kwa wale waliotimiza miaka 18 tangu uchaguzi wa 2017. Mnamo Juni 21, IEBC ilitangaza rejista iliyosahihishwa ya wapigakura, ambayo ilionyesha vijana wa umri wa miaka 18 hadi 34 walikuwa asilimia 39.84 ya wapigakura, asilimia 5.27 chini ya mwaka wa 2017, huku vijana wa kiume wakipungua kwa asilimia 2.89 na vijana wa kike kupungua kwa asilimia 7.75. Ujumbe  ulibainisha kuwa ujumbe juu ya usajili haukuwalenga vijana moja kwa moja na haukujaribu kutumia mifumo ya kidijitali wakati wa uhamasishaji. Wahojiwa katika Mombasa, Nakuru, Nairobi na Kisumu walifahamisha Ujumbe kwamba magenge ya vijana walikodiwa na wagombea ili kuvruga  hafla za kampeni za wapinzani au kuwazuia wapiga kura kupiga kura wakati wa mchujo. Kuanzia Juni 14, mashirika ya vijana yaliwafunza dazeni nyingi za wapigakura vijana katika ngazi ya kaunti kuhusu mfumo wa kisheria wa uchaguzi na taratibu za upigaji kura wakishirikiana na Kamati ya Kuratibu ya Vijana ya IEBC. Mpango huu ulifaulu zaidi ya mpango wa IEBC wa elimu kwa wapigakura ulioanza katikati ya Julai. IEBC pia iliidhinisha kwa mara ya kwanza mamia ya wanafunzi kutoka Chama cha Amani cha Wanafunzi wa Vyuo Vikuu na Vyuo vya Kenya kuwa waangalizi wa uchaguzi.

Ushiriki wa watu wenye ulemavu: Sheria ya Uchaguzi inatoa rai kwamba angalau watu wawili wenye ulemavu wateuliwe kuwakilisha maslahi ya watu wenye ulemavu katika Seneti, Bunge la Kitaifa na katika Mabunge yote ya Kaunti. Hata hivyo, vyama vya siasa vimemeshindwa kuhakikisha kuwa watu wenye ulemavu wanatambuliwa, kufanywa wanachama na kuungwa mkono ili kushiriki ipasavyo katika michakato ya ndani ya chama. na inaposhirikishwa, juhudi hizo kwa kiasi kikubwa zimekuwa za kiishara.. Kulingana na ORPP,  ni chini ya asilimia moja ya wanachama wa chama ambao ni watu wenye ulemavu. Kufuatia kuchapishwa kwa orodha za uteuzi wa vyama vya siasa mnamo Julai 27, mashirika ya watu wenye ulemavu yalikosoa vyama vya siasa kwa kutofuata sheria kwa kuwateua watu ambao hawajasajiliwa na Baraza la Kitaifa la Watu Wenye Ulemavu.

Jambo la kuvutia ni kwamba  IEBC kwa mara ya kwanza ilirekodi hali ya ulemavu wa wapigakura wapya na aina ya ulemavu waliokuwa nao kwenye rejista ya wapigakura na kuruhusu wapigakura wazee wenye ulemavu kusasisha hali zao za ulemavu. Kulingana na IEBC, watu wenye ulemavu  ni asilimia 8.7 ya wapiga kura wote waliosajiliwa. Aidha, Tume ilizindua mipango kadhaa ya kuwezesha kujumuishwa kwa watu wenye ulemavu katika mchakato wa uchaguzi, ikiwa ni pamoja na kutengeneza toleo la Braille la nyenzo za elimu ya mpiga kura na mafunzo ya Wakalimani wa Lugha ya Alama ya Kenya kama waelimishaji wa wapiga kura[6].Wahojiwa, ikiwa ni pamoja na Kamati ya Uratibu wa Ulemavu na Ujumuishi ya IEBC, walishabikia mipango hii lakini wakaikosoa Tume kwa kutotumia mbinu shirikishi zaidi katika kufanya maamuzi na kwa kutegemea miradi ya dharura badala yake. kuliko utungaji sera wa muda mrefu. Vile vile, vikiwa kwenye orofa ya kwanza, vituo vingi vya kupigia kura bado havina njia panda kuwezesha wapigakura walio na uwezo mdogo wa kutembea[7]. Hata hivyo, maafisa wasimamizi na wapiga kura wengine wa muda walitoa usaidizi wa kutosha kwa wapigakura wenye ulemavu, kwa mujibu wa kanuni ya 72 ya Kanuni za Uchaguzi (Mkuu) za mwaka 2012.

Mazingira ya Habari

Kenya ina mazingira anuwai ya vyombo vya habari na huria yenye magazeti, redio na televisheni nyingi zinazoripoti kuhusu sera na maslahi ya taifa. Redio ndiyo njia inayotumiwa zaidi na watu wengi zaidi na inafikiwa kwa kiasi kikubwa katika maeneo ya mashambani kupitia vituo 54 vya redio vya lugha za kienyeji vinavyotangaza katika lugha 19 tofauti. Kenya pia inadumisha mojawapo ya viwango vya juu zaidi vya kupenya kwa mtandao barani Afrika (asilimia 85.5) ambayo imekuza maendeleo ya vyombo vya habari vya mtandaoni. Kuanzishwa kwa utangazaji wa televisheni ya terrestrial mwaka wa 2015 kumeongeza kwa kiasi kikubwa idadi ya chaneli za televisheni. Ingawa mazingira ya vyombo vya habari nchini Kenya ni tofauti, mashirika mengi ya vyombo vya habari (asilimia 83) yanamilikiwa na wanasiasa au watu binafsi wenye mielekeo ya upendeleo. Katika kipindi cha kabla ya uchaguzi, kampeni ya Kenya Kwanza mara kwa mara ilishutumu vyombo vya habari vinavyomilikiwa na watu binafsi kwa utangazaji wa upendeleo. Aidha, wasiwasi kuhusu umiliki wa vyombo vya habari umeimarishwa na uidhinishaji wa hali ya juu kama vile mmiliki wa Royal Media Services, ambaye inashikilia asilimia 60 ya soko la vyombo vya habari nchini Kenya, kutangaza hadharani kumuunga mkono Odinga.

Kufuatia malalamiko ya utangazaji usio wa haki kwa vyombo vya habari, mnamo Juni 24, Baraza la Vyombo vya Habari la Kenya (MCK) lilitoa tathmini ya kiasi cha taarifa za matukio kwenye vyombo vya habari kuhusu wagombea 17 wanaowania urais katika kipindi cha Aprili hadi mwanzoni mwa Juni. Kwa wagombea wanne walioidhinishwa Odinga alikuwa na asilimia 61.24 ya jumla ya matangazo yote ya vyombo vya habari, akifuatiwa na Ruto aliyepata asilimia 38.2, George Wajackoyah aliyepata asilimia 0.54 na David Mwaure aliyepata asilimia 0.02. Odinga alikuwa na sehemu kubwa ya utangazaji kuliko Ruto katika redio, televisheni na vyombo vya habari vya magazeti. Kwa wagombea wote wanne walioidhinishwa, redio iliwakilisha sehemu kubwa zaidi ya utangazaji wa vyombo vya habari.

Katiba ya 2010 ilipunguza adhabu za serikali kwa uchochezi, matamshi ya chuki, propaganda dhidi ya serikali wakati wa vita na uvunjaji wa faragha. Walakini, mnamo 2018, bunge lilipitisha mswada wa kupambana na habari ghushi ambapo iliipa serikali mamlaka iliyopanuliwa katika kuamua ni nini kinachostahili kuwa habari potofu au taarifa za uongo. Wakati serikali ilianza kutoa shinikizo la haraka kwa taasisi za vyombo vya habari na wanablogu wakati utangazaji wao ulikuwa wa kukosoa au kufichua hadithi za aibu, matukio kama hayo ya udhibiti yamepungua. Kwa watu wengi nchini Kenya, mitandao ya kijamii imekuwa chanzo kikuu cha habari zinazohusiana na uchaguzi na uwanja mzuri wa kampeni za kisiasa.

Kipindi cha kampeni kimekumbwa na uenezaji mpya wa habari potofu kuenea kupitia mitandao ya kijamii. Tiktok (ambayo ilikuwa programu ya kijamii iliyopakuliwa zaidi mwaka wa 2021 nchini Kenya) iliibuka kama jukwaa jipya lenye nguvu la ujumbe wa chuki, migawanyiko na uwongo. Video zilizohaririwa zilizo na manukuu yaliyotafsiriwa kimakosa, hotuba zilizohaririwa, taarifa potofu zinazohusishwa na watu binafsi na taasisi, na picha kwenye mikutano ya hadhara ili kuathiri mitazamo ya umaarufu zote zimetumika. Lugha za kienyeji, ambazo huepuka kutambuliwa na kanuni za utambuzi wa vitisho kwenye mitandao ya kijamii, zilitumika kama zana za kutuma ujumbe kwa siri na matamshi ya chuki ambayo baadhi yao yalilenga wanawake au yalitumia mashambulizi ya kikabila. Wakati NCIC ilitoa orodha ya matamshi ya chuki (hatelex) ya maneno 23 ambayo hayafai kutumiwa na wanasiasa au watu wengine, yameonekana kutofaa kuwafanya watendaji wa kisiasa kuawajibika wakati maneno hayo yanatumika. Waandishi wa habari pia walikuwa walengwa wa ghasia katika kipindi cha kabla ya uchaguzi, hasa katika ngome ambazo wamiliki wa vyombo vya habari wameonyesha kuunga mkono upande wa upinzani.

Miungano yote miwili ya kisiasa ilitumia vikundi vingi vya watu bandia kupitia jukwaa la Facebook kusambaza ujumbe uliolenga kudhalilisha wapinzani wao. Mada zilihusu sifa za kitaaluma au ukosefu wake, uhusiano wa enzi ya Moi na Ruto na mgombea mwenza wake na kumchora Odinga kama sehemu ya nasaba za Kenya. Mashambulizi mengi yaliyolengwa yalifichua mashine ya propaganda ya mtandaoni iliyoratibiwa sana inayoeneza simulizi zinazounga mkono al-Shabaab na Dola ya Kiislamu na kuashiria pengo kubwa katika suala la udhibiti wa maudhui yasiyo ya Kiingereza katika majukwaa ya mitandao ya kijamii. Kwa kujibu, majukwaa huru ya kukagua ukweli, kama vile Pesa Check na Africa Check yaliongeza juhudi zao. Mawasiliano hafifu ya IEBC na ukosefu wa mkakati wazi wa kushughulikia habari potofu za uchaguzi, haswa katika jukwaa la kidijitali, iliathiri uwezo wao wa kupunguza ipasavyo habari potofu, kama vile nadharia za njama za ushirikiano kati ya IEBC na Kenya Kwanza ili kuvuruga uchaguzi.

Ushiriki wa Asasi za Kiraia

Licha ya kukabiliwa na vikwazo vya ufadhili, mashirika ya kiraia ya Kenya yalikuwa mhusika mkuu katika vipengele kadhaa vya mchakato wa uchaguzi wa 2022. IEBC iliidhinisha takriban makundi 115 kutekeleza mipango ya elimu ya wapigakura pamoja na waangalizi zaidi ya 15,000 kufuatilia mchakato wa uchaguzi na kushiriki katika PVT na Kundi la Waangalizi wa Uchaguzi (ELOG). Kwa mara ya kwanza, mamia ya wanafunzi kutoka Chama cha Amani cha Wanafunzi wa Vyuo Vikuu na Vyuo vya Kenya waliidhinishwa kuwa waangalizi wa uchaguzi. Zaidi ya hayo, juhudi za amani na kupunguza vurugu zilijumuishwa lakini hazikujikita tu katika taratibu za onyo na majibu ya mapema, usaidizi kwa wapatanishi, uchanganuzi wa migogoro ya uchaguzi, usimamizi wa utaratibu wa umma na ufuatiliaji wa matukio ya wakati halisi. Juhudi pia zilifanywa kuwajumuisha wanawake katika shughuli za kujenga amani kupitia mabaraza mahususi ya wanawake, kuajiri wanawake kama waangalizi wa tahadhari za mapema na viashiria vilivyoanzishwa, na mgao bajeti. Kwa mara ya kwanza nchini Kenya, timu ya waangalizi wa uchaguzi wa SGBV (E-SGBV), wote watetezi wa haki za binadamu, walitumwa kote nchini na FIDA-Kenya.

Siku ya Uchaguzi

Mnamo tarehe 9 Agosti, wapiga kura walipiga kura sita tofauti kwa: rais na makamu wa rais; wajumbe wa Bunge; wawakilishi wa wanawake Bungeni; wajumbe wa Seneti; magavana wa kaunti; na wajumbe wa bunge za Kaunti. Rais anachaguliwa kwa kupata asilimia 50 pamoja na kura moja ya kitaifa na angalau asilimia 25 ya kura katika kaunti 24 kati ya 47. Ikiwa hakuna mgombeaji atapita kiwango hiki, rudio la pili litafanyika kati ya wagombea wawili watakaopata kura nyingi zaidi katika awamu ya kwanza.

Ufunguzi: Mazingira ya jumla kwa ujumla yalikuwa tulivu na ya amani huku waangalizi wakibaini foleni za wapiga kura waliokuwa na hamu. Matukio machache ya kuchelewa kufunguliwa kwa vituo vya kupigia kura yalisababisha misururu mirefu kwenye vituo vya kupigia kura, ingawa haya hatimaye yalitatuliwa vituo vya kupigia kura vilipofunguliwa baadaye asubuhi. Nyenzo zinazohitajika zilipatikana katika vituo vyote vya kupigia kura vilivyoangaliwa ikiwa ni pamoja na vifaa vya KIEMS. Wakati wa mchakato wa ufunguzi, masanduku ya kura yalionyeshwa kuwa tupu kabla ya kufungwa katika vituo vyote vilivyoangaliwa. Timu zote isipokuwa tatu ziliripoti kwamba afisa msimamizi aliondoa kijitabu cha pili kati ya viwili vya Fomu ya Kutangaza Matokeo ya Uchaguzi ya urais (fomu 34A) na kuifunga kwa bahasha isiyoweza kuchezewa.

Upigaji Kura: Waangalizi walibaini kutofautiana katika kufuata taratibu za utumiaji wa rejista ya wapigakura iliyochapishwa katika vituo vya kupigia kura. Katika baadhi ya vituo, rejista iliyochapishwa ilitumiwa kama uthibitishaji wa pili wa utambulisho wa wapigakura baada ya kuthibitishwa kupitia kwa kifaa cha KIEMS lakini katika vituo vingi vya kupigia kura waangalizi walibaini kuwa rejista iliyochapishwa haikutumika licha ya kuwepo.. Waangalizi pia walibainisha kuwa matumizi ya rejista iliyochapishwa yalionekana kuwa ya kawaida hasa mwanzoni mwa upigaji kura na kupungua siku nzima. Nyenzo zinazohitajika zilipatikana katika vituo vyote vya kupigia kura vilivyoangaliwa, ikijumuisha vifaa vya KIEMS ambavyo kwa ujumla vilifanya kazi vyema siku nzima. Hata hivyo, waangalizi wachache walibaini kuwa baadhi ya wapiga kura hawakuweza kutambuliwa kibayometriki hasa wazee na wafanyakazi wa kazi za mikono hata ingawa waliweza kutambuliwa kupitia utafutaji wa alphanumeriki kwenye kifaa cha KIEMS.

Maafisa wasimamizi kwa ujumla walikuwa na ujuzi na weledi katika majukumu waliyotwikwa. Waangalizi pia walibaini ushiriki wa vijana kama maafisa wa upigaji kura. Waangalizi wengi walibaini kuwa maafisa wa usalama walidumisha utulivu na usalama siku nzima. Waliweza; kusimamia mistari mirefu na hawakusababisha taharuki kwa raia. Wagombea na maajenti wa vyama walikuwepo kwa wingi katika vituo vya kupigia kura, hasa kutoka vyama vikuu viwili vya siasa na wagombea huru, na walishiriki kikamilifu katika majukumu yao. Katika matukio mengi, waangalizi wa raia na wa kimataifa waliombwa kutoa nyaraka za ziada pamoja na kuhitajiwa kula kiapo cha usiri kabla ya kuruhusiwa kuingia kwenye vituo vya kupigia kura.

Katika baadhi ya vituo vya kupigia kura vilivyoangaliwa, vituo vya kupigia kura viliwekwa huku migongo ya wapigakura ikitazamana na makarani ambao wangeweza kuona jinsi wapiga kura wanavyoweka alama kwenye kura jambo ambalo lilihatarisha usiri wa kura. Baadhi ya waangalizi pia walibaini kuwa maajenti wa vyama walishuhudia usaidizi wa kupiga kura miongoni mwa wapigakura waliohitaji msaada hata katika hali ambapo mpiga kura alikuwa na msaidizii wake. Zaidi ya hayo,  kufika katika vituo vya kupigia kura na watu wenye ulemavu kulikuwa changamoto . Sio viingilio vyote vya vituo vya kupigia kura vilivyofikiwa na watu wanaotumia viti vya magurudumu wala hapakuwepo na makao ya wapiga kura wenye ulemavu wa macho kama vile folda za kugusa kura katika vituo vya kupigia kura vilivyoangaliwa. Hata hivyo, waangalizi wengi walibainisha kuwa watu wenye ulemavu, wanawake wajawazito, akina mama walio na watoto wachanga na wazee walipewa kipaumbele katika foleni ya kupiga kura.

Kuhesabu: Mchakato wa kuhesabu kura katika vituo vya kupigia kura ulifanyika kulingana na utaratibu.  Kura za rais ndizo zilihesabiwa  kwanza   na kufuatiwa na mjumbe wa Bunge la Kitaifa, mjumbe wa Bunge la Kaunti, Seneta,mwanamke mwanachama wa Bunge la Kitaifa na hatimaye uchaguzi wa ugavana. Kulingana na taratibu, karatasi za kupigia kura zilizowekwa kwenye sanduku lisilo sahihi zilitangazwa kuwa “zimepotea” na kukataliwa. Ingawa hili halikuathiri idadi kubwa ya kura, ilisababisha baadhi ya karatasi halali za kupigia kura kukataliwa na kufanya upatanisho wa matokeo ya kituo rasmi kuwa changamoto zaidi. Maajenti wa vyama walipewa mara kwa mara nakala za matokeo rasmi ya urais ya fomu 34A. Hata hivyo, nakala za matokeo rasmi ya urais hazikubandikwa kwenye vituo vya kupigia kura kwa umma kinyume na chaguzi zilizopita. Kufikia asubuhi ya Agosti 11, IEBC ilikuwa imeweka nakala  zaidi ya asilimia 99 yafomu 34A ya matokeo ya urais kutoka vituo 46,229  vya kupigia kura  kwenye tovuti yake.


[1] Mijadala miwili ya urais ilipangwa tarehe 26 Julai. George Wajackoyah wa Roots Party alisusia mjadala mwingine. Alipaswa kukabiliana na David Mwaure Waihiga wa Chama cha Agano.

[2] Mashariki mwa Mji wa Nakuru, waangalizi wa  raia walishuhudia mbunge wa sasa  akigawa Ksh 300 kwa nyumba  nyingi katika wadi tano za eneobunge hilo kwa siku nyingi. Katika eneo la Kisumu ya Kati, IEOK ilishuhudia mgombeaji wa ODM katika bunge la kaunti akigawa Ksh 300 kwa wafuasi kwenye mkutano mdogo wa wadi ya Kondele.

[3] Mgombea mwenza wa Urais Rigathi Gachagua alidai mnamo Julai 5 kwenye ukurasa wake wa Facebook kwamba machifu wa eneo hilo waliitwa na Naibu Kamishna wa Nyeri na kuamriwa kumkaribisha mgombeaji urais wa Azimio Raila Odinga kwenye mkutano wa kutafuta kura huko Karatina. Machifu wa mitaa ni watumishi wa umma na hivyo wamezuiwa kushiriki katika shughuli za kampeni  kwa mujibu wa Kifungu cha 23 cha Sheria ya Uongozi na Uadilifu (2012).

[4]  UWIANO, iliyoanzishwa mwaka wa 2010, ni jukwaa la umma la kuwashirikisha Wakenya katika kuongeza sauti zao katika juhudi za kukuza amani nchini Kenya

[5] Mnamo Juni 6, Mbunge wa Mugirango Kusini Silvanus Osoro, ambaye anajihusishaa na UDA, alimkosoa Martha Karua kwa  maumbile yake ya kimwlili i na hali yake yakuwa katika ndoa. Kadhalika, mgombea wa kiti cha ugavana wa ODM Gladys Wanga (Homa Bay) na mgombea wa ODM katika kiti cha uwakilishi wa  mwanamke katika Bunge la Kitaifa Ruth Odinga (Kisumu) walikabiliwa na mashambulizi ya kijinsia mtandaoni kutoka kwa wafuasi wa wapinzani wao.

[6] Wakalimani hawa walitarajiwa kuelimisha baadhi ya wapigakura 206,000 waliosajiliwa na wenye ulemavu wa kusikia. Ili kufikia lengo lake, programu ilitumia mtambo wa ‘assistAll’ (Tumikia wote) kuunganisha watumiaji wenye ulemavu wa kusikia na waelimishaji wa wapigakura wa lugha ya ishara, ambao walijibu maswali yoyote kuhusu mchakato wa uchaguzi au taratibu za kupiga kura kwenye  Video.

[7] DICC ilichora sampuli ya vituo vya kupigia kura katika kaunti 10 ambapo wapigakura wa PWD wamesajiliwa kulingana na rejista iliyokaguliwa ya IEBC ya wapiga kura. Zoezi la uchoraji ramani lililenga kuwafahamisha wapiga kura wenye ulemavu aina ya usaidizi wanaopaswa kutarajia ndani ya kituo chao cha kupigia kura.

Up ArrowTop